Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli
amemuagiza Waziri na Katibu Mkuu katika Ofisi ya Tawala za Mikoa na
Serikali za Mitaa (TAMISEMI) kusitisha mara moja utekelezaji wa zoezi la
kuwaondoa wafanyabiashara wadogo maarufu kwa jina la Machinga katika
Jiji la Mwanza pamoja na mikoa mingine mpaka hapo mamlaka husika
zitakapokamilisha maandalizi ya maeneo watakapohamishiwa na kwa
kuwashirikisha wamachinga wenyewe.
Rais Magufuli akiwa na Makamu wa Rais Mhe. Samia Suluhu Hassan ametoa
agizo hilo leo tarehe 06 Desemba, 2016 Ikulu Jijini Dar es Salaam huku
akionya kuwa kiongozi yeyote ambaye hayupo tayari kutekeleza agizo hilo
aachie ngazi.
"Kumeibuka tabia ya Wakuu wa Mikoa, Wakuu wa Wilaya na
Wakurugenzi kuwafukuza Wamachinga bila utaratibu wowote wa wapi
wanawapeleka na wakati mwingine wanapelekwa maeneo ya mbali ambayo
hayafai hata kwa kufanya biashara, wakati mwingine wanawafukuza
wachimbaji wadogo kwenye maeneo wanayofanya shughuli zao na pia
wanawafukuza wafugaji katika maeneo wanayolisha mifugo yao, hili sio
sawa.
"Sipendi Wamachinga wafanye biashara kwenye hifadhi ya
barabara lakini hakuna sheria katika nchi hii inayosema mtu wa biashara
ndogondogo au Mmachinga hatakiwi kukaa katikati ya mji, tukianza kwenda
kwenye utaratibu wa namna hiyo maana yake tunaanza kutengeneza madaraja
ya Watanzania, kwamba kuna Watanzania fulani wa daraja fulani wanapaswa
kukaa katikati ya mji na Watanzania wa daraja fulani hawatakiwi kukaa
katikati ya mji, huo sio mwelekeo wetu na wala Ilani ya Uchaguzi ya
Chama Cha Mapinduzi ambayo mimi na wewe (Makamu wa Rais) tulipita
kuinadi, haisemi tutengeneze madaraja ya watu wanaostahili kukaa mjini
na wengine hawastahili kukaa mjini, sasa nimeona hili nilizungumze na
nataka kulirudia kwa mara ya mwisho" amesema Rais Magufuli.
Dkt. Magufuli ameelekeza kuwa Wamachinga waliondolewa katika maeneo
yao Jijini Mwanza waachwe waendelee na shughuli zao mpaka hapo
Halmashauri ya Jiji la Mwanza itakapokamilisha maandalizi ya mahali
watakapohamishiwa na kwa kuwashirikisha Wamachinga wenyewe.
"Narudia na hii ni mara ya mwisho, kawaambieni hata
Wamachinga wa Mwanza warudi kwenye maeneo yao mpaka watakapowatengenezea
utaratibu mzuri, Kigamboni hapa palikuwa na wamachinga eneo fulani
wamehama vizuri kweli, wakatengenezewa miundo mbinu yao katika soko lao
na sasa hivi wanafanya kazi vizuri, na waliwashirikisha viongozi wa
Wamachinga, lakini Mwanza imekuwa ni amri tu na wengine wanatumia hata
msemo wa Hapa Kazi Tu, mimi sikusema msemo wa Hapa Kazi Tu wa namna
hiyo, nadhani mmenielewa" amesisitiza Rais Magufuli
alipokuwa akiwaekeleza Naibu Waziri wa TAMISEMI Mhe. Suleiman Jafo na
Katibu Mkuu TAMISEMI Mhandisi Mussa Iyombe.
Wakati huo huo, Rais Magufuli ameagiza Wizara ya
Nishati na Madini kusitisha mara moja zoezi la kuwaondoa wachimbaji
wadogo katika Kijiji cha Nyaligongo kilichopo katika Kata ya Mwakitolyo
Mkoani Shinyanga na badala yake wachimbaji hao waachwe waendelee na
shughuli zao, na leseni ya mwekezaji anayedai eneo hilo ni lake
aondolewe.
"Wale waliofukuzwa Shinyanga wabaki palepale, kama ni
leseni ya huyo mwekezaji ifutwe, Mhe. Makamu wa Rais fuatilia hili,
mweleze Waziri wa Nishati na Madini, waache kufukuza wananchi
hovyohovyo, wale wanapata riziki yao, wanasomesha watoto wao lakini
wanafukuzwa tu.
"Na hizi ndio ajira zenyewe, tulisema tunatengeneza
ajira, wewe mwekezaji ni mmoja unakwenda kuwafukuza watu 5,000?
haiwezekani na wala haingii akilini" amesisitiza Rais Magufuli.
Rais Magufuli amekemea vitendo vya wawekezaji wakubwa kupewa maeneo
ambayo wachimbaji wadogo wanaendesha shughuli zao tena kwa mtindo kwa
kutengeneza nyaraka zinaonesha mwekezaji husika alipewa eneo hilo kabla
ya wachimbaji wadogo na kusisitiza kuwa mchezo huo hautavumiliwa.
Hata hivyo Rais Magufuli amesema maagizo yake hayana maana kuwa
Wamachinga na Wachimbaji wadogo waendeshe shughuli zao kwa kuvunja
sheria bali wazingatie sheria na Mamlaka zisiwanyanyase watu wanyonge
Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Dar es Salaam
06 Desemba, 2016
No comments:
Post a Comment